Kocha
mkongwe wa mchezo wa kuogelea nchini Ferick Kalengela amepinga uteuzi
wa muogeleaji wa kike wa Tanzania, Magdalena Moshi kuiwakilisha nchi
katika mashindano ya Olimpiki kupitia tiketi ya Nafasi za Upendeleo
iliyolewa na waandaaji.
Chama
Cha Kuogelea nchini (TSA) kiliwakilisha jina la mchezaji huyo pamoja na
muogeleaji wa kiume, Hilal Hemed Hilal kuiwakilisha nchi kwa njia ya
tiketi hiyo, lakini Kalengela amesema kumjumuisha Magdalena ni kinyume
na matarajio yao hata kama Shirikisho la Mchezo wa kuogelea Duniani
(Fina) kuweka vigezo vyake.
Fina
iliweka vigezo kuwa waogeleaji walioshiriki mashindano ya kuogelea ya
Dunia yaliyofanyika mwaka jana nchini Kazan kuwa ndiyo wanaopaswa kuwepo
katika nafasi ya kuiwakilisha nchini kwa nafasi ya upendeleo. Sonia
hakuweza kushirki mashindano hayo ambayo Tanzania iliwakilishwa na
wachezaji watatu, Hilal, Ammaar Ghadiyali na Magdalena.
Kalengela
alisema kuwa vigezo hivyo havipaswi kutumika kwa uteuzi wa waogeleaji
wa Tanzania kwani Magdalena mbali ya kuiwakilisha nchi katika mashindano
ya Kazan yaliyofanyika kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka jana,
hajawahi kushiriki mashindano yoyote hapa nchini kuthibitisha ubora
wake.
Kocha
huyo mkongwe nchini alisema kuwa muogeleaji nyota wa kike hapa nchini,
Sonia Franco Tumiotto ndiye anapaswa kupewa nafasi hiyo hata kama
hajashiriki mashindano ya dunia, lakini matokeo yake ya hapa nchini na
nje ya nchi yanampa nafasi.
Alifafanua
kuwa Magdalena ambaye anasoma na kuishi nchini Australia, hakuweza
kufika mashindano ya Taifa ambayo Sonia alikuwa mshindi wa jumla kwa
kushinda medali 10 za dhahabu huku akivunja rekodi 10 mbalimbali za
taifa.
“Sonia
pia ameweza kushinda medali tatu katika mashindano ya kufuzu Olimpiki
ya Dubai akiwa mmoja wa waogeleaji wanne wa timu ya Taifa, alishinda
medali ya dhahabu moja na shaba mbili, Magdalena hakushiriki katika
mashindano hayo, ilikuwa kazi rahisi tu kwa TSA kupendekeza jina la
Sonia kwa kutoa sababu za kiufundi ili aweze kupewa nafasi hiyo, ni
kweli kuwa Sonia pamoja na kuwa hajashiriki mashindano ya Dunia, lakini
kwa sasa ndiye muogeleaji namba moja nchini kwa upande wa wanawake,”
alisema Kalengela.
Alisema
kuwa hata ukilinganisha matokeo ya Sonia na Magdalena, utapata jibu
kuwa Sonia ni zaidi ya muogeleaji huyo kwa sekunde 1.30 kwa staili ya
freestyle mita 50. “Je TSA haijaona hili, je kama ingetokea mmoja wa
waogeleaji amepata dharura, nafasi hiyo ingepotea? Tuepuke mazoea na
sasa tunatakiwa kwenda kwa uhalisia, kufanya hivi ni kupoteza ushindani
wa mchezo na kuwavunja moyo waogeleaji na wadau hasa wazazi,” alisema.
Katibu
Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi alikiri kupokea
jina la Magdalena na Hilal na kuweka wazi kuwa kazi ya Kamati ni kupokea
na wala si kuchagua.
Muogeleaji
wa Tanzania Sonia Tumiotto (wa kwanza kushoto) akipokelewa kwa shangwe
Katibu Mkuu wa Chama Cha Kuogelea nchini (TSA), Ramadhan Namkoveka na
Katibu Mkuu wa klabu yake (Dar Swim Club), Inviolata Itatiro mara baada
ya kuwasili kutoka Dubai alipokwenda kutafuta tiketi ya kufuzu
mashindano ya Olimpiki. Pamoja na kufanya vyema, muogeleaji huyo
hajapewa nafasi ya kuiwakilisha nchi kwa njia ya upendeleo kutokana na
kukosa vigezo vya Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (Fina) ambazo
zinawapa nafasi waogelaji wote walishindana mashindano ya Dunia ya
Kazan.
“Awali
TSA ilileta majina matatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja,
nikawaandikia barua kuwataka watume majina mawili kwa mujibu wa
taratibu, nikaletewa Hilal na Magdalena, siwezi kufanya lolote, hayo ni
masuala ya chama na shirikisho lao, siwezi kuingilia,” alisema Bayi.
Akijibu
madai hayo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TSA, Amina Mfaume alikiri kuwa
Magdalena hajashiriki mashindano ya mwaka huu ya Taifa yaliyofanyika
kwenye bwawa la Hopac kutokana na kukabiliwa na mitihani, lakini uteuzi
wake umetokana na majina yaliyoletwa na Fina.
Amina
alisema kuwa hawahampendelea Magdalena katika uteuzi huo kwani vigezo
vya Fina ndivyo vimempa nafasi Magdalena na wao hawawezi kwenda kinyume.
“Tunafuatilia
maendeleo Magdalena ya huko Australia kupitia mwalimu wake, hata Sonia
ambaye tupo Uingereza naye tunafuatilia maendeleo yake, hivyo hakuna
wasiwasi wa ushiriki wa Magdalena, ni muogeleaji mzuri, hajapendelewa, ”
alisema Amina.
Muogeleaji
wa Tanzania Sonia Tumiotto (katikati) akiwa katika picha ya pamoja
baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Dubai. Sonia
alitwaa medali tatu katika mashindano hayo pia yaliandaliwa kwa ajili
ya kutafuta tiketi za kufuzu Olimpiki Dubai.
0 comments:
Post a Comment