WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
viongozi wa dini kushirikiana na Serikali katika
kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazoikabili zikiwemo za rushwa, ufisadi na
matumizi mabaya ya fedha za umma.
Amesema siku zote kumekuwa na ushirikiano
mzuri kati ya Serikali na Asasi mbalimbali ikiwa
ni pamoja na madhehebu ya Dini katika
kuwapatia huduma za kijamii kama vile, afya,
elimu, maji, utunzaji wa mazingira na nyingi
nyingine.
Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo jana
mchana (Jumapili, Juni 12, 2016) wakati
alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dk. John
Magufuli katika Ibada ya kuwekwa wakfu na
kusimikwa kuwa Mhashamu Askofu Flavian
Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki
Geita.
“Serikali inatambua jitihada kubwa zilizowekwa na
Kanisa Katoliki katika Jimbo hili la Geita na
Tanzania kwa ujumla hivyo wito wangu kwa Baba
Askofu na Waumini wa Kanisa kwa ujumla wenu
ni kuwaomba muendelee na kazi hii nzuri ya
kutoa huduma muhimu kwa jamii,” alisema.
Alisema maendeleo ya nchi yanawategemea
wote hivyo ushirikiano kati ya Kanisa na
Serikali utawezesha maendeleo ya Taifa
kupatikana kwa kasi zaidi na kunufaisha
wananchi wote.
Waziri Mkuu alisema jukumu la Serikali ni
kuweka mazingira wezeshi ambayo yatasaidia
Mtanzania kujikomboa na umaskini na kwamba
kazi kubwa ya viongozi wa dini kuunganisha
jamii na wala siyo kuwatenganisha.
Hata hivyo Waziri Mkuu alisema kinachotakiwa
kufanywa na wote ni kumwuomba Mwenyezi
Mungu awawezesha kuwaelewa viongozi
walioko madarakani na kutii maelekezo
yanayotolewa kwani hata vitabu vya dini
vinaelekeza kutii mamlaka.
Alisema iwapo waumini watatii na kuzingatia
mafundisho ya kiroho yanayotolewa na viongozi
wao wa dini ni dhahiri kwamba yatajenga imani
miongoni mwao na upendo utatawala katika
jamii nzima.
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea
kushirikiana na Madhehebu yote katika
kuwahudumia Watanzania wote bila ubaguzi,
hivyo aliwasihi waendelee kuwekeza katika
huduma za jamii ikiwemo Shule, Vyuo, Zahanati
kwa kuwa wana jukumu la kushirikiana kwa
pamoja kujenga taifa.
Wakati huo huo Waziri Mkuu aliwaomba wote
kwa pamoja waunge mkono juhudi za
Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli katika
kupambana na uzembe, ubadhirifu na wote
wanao kiuka maadili ya utendaji wa kazi.
Kwa upande wake Askofu Renatus Nkwande wa
Jimbo la Bunda ambaye alikuwa msimamizi wa
Kitume Jimbo Katoliki Geita amewaomba
waumini kumpa ushirikiano Askofu mpya wa
jimbo hilo.
IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JUNI 12, 2016.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment