Comments


Polisi Jijini Mwanza Wapambana na Majambazi kwa Saa 16.....


Watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi,wameuawa katika majibizano ya risasi na askari polisi mkoani Mwanza,alfajiri ya kuamkiajana jumapili katika mapango ya mlima wa Utemini yaliyopo kata ya Mkolani jijini Mwanza.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza Ahmed Msangi,amewataja majambazi waliouwa katika majibizano ya risasi usiku kucha kuwa ni Omar Francis Kitaleti mkazi wa Nyegezi Kona,said Khamis Mbuli maarufu kama fundi bomba mkazi wa bugarika na jambazi mwingine ambaye jina lake bado halijafahamika.

Amesema majambazi hayo yalikuwa yamejificha kwenye mapango ya mlima wa Utemini kabla ya askari polisi kufanikiwa kuyaua.

Jambazi mmoja aliyeuawa ambaye hajafahamika jina lake mwenye umri kati ya miaka 20 hadi 25 alikuwa akiwashambulia polisi kwa kutumia bastola ambapo baada ya polisi kumpiga risasi walimpekua na kumkuta akiwa na bastola aina ya Chinese,iliyokuwa na risasi tatu ndani ya magazine,huku majambazi wengine waliokuwepo kwenye mapango hayo wakiendelea kujibishana kwa risasi na askari polisi.

Kamanda Msangi ameongeza kwamba Ijumaa Juni 3,askari polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama,walimkamata Omar Francis Kitaleti kwa jina maarufu kiberiti,mkazi wa Nyegezi Kijiweni ambaye alikuwa akituhumiwa kuhusika katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwenye maduka ya M-pesa,Tigo Pesa na Airtel money jijini Mwanza ambaye baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika katika matukio hayo na aliwataja wenzake anaoshirikiana nao na mahali walipojificha.

Amesema ilipotimu majira ya saa kumi na moja kamili jioni siku ya Jumamosi Juni 4,polisi walifika katika mlima huo na walipoyakaribia mapango hayo ghafla walianza kushambuliwa kwa risasi na majambazi waliokuwa wamejificha ndani ya mapango hayo.
Omary Francis Kitaleti @Kiberiti, mmoja wa majambazi aliyeuawa na wenzake kwa risasi.

Katika mapambano hayo ya risasi na askari polisi,risasi hizo ziliweza kumpata jambazi mwenzao aitwaye Omary Francis Kitaleti aliyekuwa anawaongoza askari polisi na kufariki dunia papo hapo, na risasi nyingine ilimjeruhi askari kwenye unyayo wa mguu wake wa kulia.

Amesema polisi kwa kutumia mbinu za medani za kivita waliweza kuzingira maeneo hayo ya mlima wa utemini hadi alfajiri ya kuamkia Jumapili Juni 5,huku wakijibishana risasi na majambazi hao na baada ya kuona yamezidiwa nguvu huku kukikaribia kupambazuka ndipo yalipoamua kuondoka ndani ya mapango hayo kwa kurusha bomu moja la kutupa kwa mkono huku yakizidisha mapigo ya risasi kwa kutumia silaha walizokuwa nazo.

Ameongeza kuwa polisi wamekamata bunduki moja aina ya SMG iliyokuwa na risasi nane na kisu kimoja.

Kamanda Msangi amesema majambazi watatu walifanikiwa kutoroka kutoka kwenye mapango hayo kuelekea maeneo ya Nyasaka na baada ya jambazi mmoja kubaini kuwa askari polisi walikua wanamfuatilia alitoa bunduki  na kutaka kuwapiga askari polisi lakini polisi waliweza kumuwahi na kumfyatulia risasi sehemu mbalimbali za mwili wake na kufariki dunia papo hapo.

Amesema askari polisi wamefanya upekuzi kwenye mapango ya mlima wa Utemini na kufanikiwa kupata vitu mbalimbali vilivyoachwa na majambazi hao ambavyo ni pamoja na risasi nne,kisu kimoja chenye damu,kofia ya kuficha uso nyeusi moja (mask),jiko la stove,masufuria ya kupikia, unga wa mahindi,sukari,dagaa,chakula kilichopikwa,ngoma mbalimbali,na simu tatu za mkononi.

Askari aliyejeruhiwa amelazwa hospitali ya rufaa ya bugando na hali yake inaendelea vizuri,polisi bado wanaendelea na msako wa kuwatafuta majambazi waliofanikiwa kutoroka.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo alitembelea kwenye mapango ya Utemini na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi katika kuwafichua wahalifu
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system