Mbunge wa jimbo la Chalinze mkoa wa Pwani Ridhiwani Kikwete alipokwenda jana kutembelea shule ya sekondari Chalinze baada ya bweni la wanafunzi wa kiume kuungua kutokana na shoti ya umeme. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
WANAFUNZI 65 wa shule ya sekondari chalinz e iliyopo Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamenusurika kifo baada ya bweni lao kuteketea kwa moto wakati wao wakiwa darasani kwa ajili ya kujisomea masomo ya usiku.
Akizungumza na MWANDISHI WA HABARI HIZI kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema tukio hilo limetokea april 17 majira ya saa 3:20 usiku .
Mkuu huyo alisema chanzo cha moto huo inadaiwa ni shoti ya umeme ambayo imesababisha moto huo kuteketeza vifaa vyote vikiwemo magodoro,vitanda,vitabu katika bweni hilo.
Mwanga akizungumzia kuhusiana na juhudi za serikali ambazo tayari wameshazichukua hadi sasa alisema wanawahifadhi wanafunzi hao katika jengo lingine la muda ambalo lilikuwa linatumika kwa chakula.
Alisema kuwa pia serikali ya mkoa imeshaanza kuwasiliana na wadau mbalimbali ambao watasaidia kununua vifaa vya ujenzi kwa kusaidiana na serikali ili kujenga bweni jingine.
“Siwezi kusema hali ni nzuri kutokana na watoto wameunguliwa vifaa vyao,ni hasara katika jengo pia kwahyo kilichopo sasa ni kumshukuru mungu kwa wanafunzi hawa kunusurika”alisema Mwanga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo Chalinze Hussein Mramba alikiri kutokea kwa tukio hilo
Alisema mkandarasi wa halmashauri ya wilaya hiyo bado anaendelea na tathmini ya miundombinu iliyoungua.
Shule ya sekondari Chalinze ina jumla ya idadi ya wanafunzi 1,151 kati yao 65 kwa sasa wameunguliwa na vitu vyao vyote hivyo kunahitajika juhudi za jamii,wadau na serikali katika kuhakikisha wanatoa msaada wa hali na mali .
0 comments:
Post a Comment