Comments


TAKUKURU YAMFIKISHA MAHAKAMANI MKUU WA SHULE KWA KUOMBA RUSHWA YA NGONO

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Singida, imemburuza mahakamani mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ukombozi mjini hapa Samwel Juma Kingu (47), kwa tuhuma ya kushawishi kupewa rushwa ya ngono.

Mshitakiwa huyo mwalimu Kingu juzi mchana alipandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini hapa.

Awali mwendesha mashitaka mchunguzi mwandamizi wa makosa ya jinai TAKUKURU mkoani hapa, Bibie Mussumi, alidai mbele ya hakimu Thysophie Tesha, kuwa mnamo Februari, 17 mwaka huu muda usiofahamika, mshitakiwa kwa makusudi alishawishi apewe rushwa ya ngono.

Akifafanua, alisema kuwa mshitakiwa Kingu alimshawishi Salima Iddi ampe ambaye alikuwa anamwombea uhamisho mdogo wake anayesoma darasa la sita, ahamie Temeke, Dar es Salaam.

Mussumi alisema mwalimu Kingu ametenda kosa hilo huku akijua wazi kitendo hicho haramu ni kinyume na kifungu 15 (1) (a) (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa no.11 ya mwaka 2007.

Mwendesha mashitaka huyo, alimsomea  mshitakiwa shitaka la pili  la kujaribu kupokea rushwa ya ngono ndani ya chumba cha nyumba ya kulala wageni ya J.M.Ferama mjini Singida.

Alisema mshitakiwa Kingu wakati wa kukamatwa, alikutwa akiwa mtupu huku Salima akiwa na nguo zake ameketi juu ya kitanda, ndipo TAKUKURU walipoingilia kati mwalimu huyo asitekeleze azma yake.

Mussumi aliiambia mahakama hiyo kwamba upelelezi bado haujakamilika na pia hana tatizo au pingamizi lolote dhidi ya kupewa dhamana mshitakiwa.

Hakimu Tesha alisema yeye hajapangiwa kesi hiyo isipokuwa amepewa ili aipangie tarehe nyingine ya kutajwa.

“Kwa hiyo, mshitakiwa mwalimu Kingu utaenda mahabusu  magereza  hadi Aprili, 18 mwaka huu, kesi yako itakapokuja kutajwa tena,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system