Mkuu wa mawasiliano wa Airtel Beatrice Singano. |
KATIKA muda wa siku 90 Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kupitia mradi wake wa fursa, msimu wa pili imefanikiwa kuwawezesha vijana zaidi ya 60 katika makundi ya ujasiriamali 11.
Uwezeshaji huo upo katika kuwapatia elimu ya ujasiriamali pamoja na kuwawezesha vitendea kazi vya kisasa ili waweze kufikia ndoto zao.
Mikoa iliyofikiwa na Airtel kupitia mradi huo wa jamii ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Kagera, Manyara na Dodoma.
Mkuu wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano alisema mikoa 6 tayari imefaidika na shilingi milioni 125 za mradi wa Airtel Fursa na bado mradi unaendelea.
Alisema Airtel kila wiki hutumia Sh milioni 20 kwa ajili ya makundi mawili au vijana wawili watakaojitokeza na kuomba kuwezeshwa na mradi wa Airtel Fursa, alisema Singano.
“Awali mwaka huu tulitenga jumla ya Sh bilioni moja kwa ajili ya kuwasaidia vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 kuweza kutumia fursa walizonazo na kujiajiri wao wenyewe pamoja na wengine, sasa pesa hizi zipo na zinawasubiri,“alieleza Singano.
Katika siku 90 wamesaidia vijana wanaojishughulisha na biashara au ujasiriamali katika utunzaji wa mazingira, ufugaji, kilimo cha kisasa pamoja na biashara mbalimbali, zikiwemo za saluni kwa wanawake, ufundi seremala, uvuvi, pamoja na bucha la nyama kwa familia.
Mpango wa Airtel Fursa unawalenga vijana walio katika umri wa miaka 18 hadi 24. Ili kijana ashiriki au kufaidika na Airtel Fursa atatakiwa kutuma ujumbe mfupi kwenda kwa namba 15626 au barua pepe kwa airtelfursa@tz.airtel.com.
0 comments:
Post a Comment