Comments


JKT NA JESHI LA MAGEREZA WAMKWAZA RAIS KWA KUTENGENEZA IDADI NDOGO YA MADAWATI.

RAIS John Magufuli, amelishukia Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) na la Magereza kwa
kutengeneza idadi ndogo ya madawati kutokana
na Sh. bilioni nne zilitolewa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili,
mwaka huu.
Akizungumza wakati wa shughuli ya
makabidhiano ya madawati hayo kwenye
viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana,
Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwake na
majeshi hayo kutengeneza madawati 53,450 tu
katika kipindi cha miezi mitatu (siku 90) tangu
fedha hizo zilipotolewa wakati wana nguvu kazi
ya kutosha.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jana jioni na
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson
Msigwa, ilieleza kuwa, madawati 61,385 ndiyo
ambayo yametengenezwa katika awamu ya
kwanza kutokana na fedha hizo za Bunge, ikiwa
ni idadi tofauti iliyosemwa na Rais mapema
kwenye hafla hiyo.
Taarifa ya Ikulu ilifafanua kuwa, madawati
mengine 60,000 yatatengenezwa kwenye
awamu ya pili.
Rais Magufuli aliongeza kuwa, ukigawa idadi ya
siku 90 kwa vyombo viwili vya JKT na
Magereza, maana yake kila chombo
kimetengeneza madawati 30,000.
Rais Magufuli alisema JKT ina kambi nyingi na
kutolea mfano za Oljoro, Makutupora, Mafinga,
Mpwapwa, Mlale na kwamba ukigawa kwa idadi
ya kambi hizo kwa madawati 30,000 unapata
wastani wa madawati 30 kwa siku, ambayo
yametengenezwa na kila kambi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wakuu wa
JKT na Magereza kuchukua jukumu hilo la
utengenezaji madawati kama vita, kwa
kuwatumia wafungwa na nguvu kazi zilizopo
katika vikosi kuharakisha utengenezaji wa
madawati.
Katika shughuli hiyo alikabidhi madawati hayo
kwa wabunge wa mikoa ya Dar es Salaam,
Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa,
Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja,
Pemba na Tanga.
Madawati hayo yalitengenezwa kutokana na
hundi ya Sh. bilioni nne iliyotolewa na Bunge na
kukabidhiwa Rais Magufuli Aprili 11, mwaka huu
kama mpango wao wa kubana matumizi.
“Natoa wito kwa vyombo vya ulinzi, JKT na
Magereza japokuwa mmetengeneza madawati
lakini mjipange katika hili, haiingii akilini, nimekaa
JKT mwaka mzima najua hamuwezi kutengeneza
madawati machache hivi,” alisema Magufuli.
“Niwaombe, chukueni hili kama jukumu la haraka,
tunahitaji madawati, ninahitaji madawati leo na
Waziri Mwinyi (Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi) yupo hapa na
kwa bahati mbaya hajaenda JKT hajui shida
tunazozipata kule, labda siku mumpeleke siku
akaone, sisi tunafahamu kule ni kazi tu,” alisema
Rais Magufuli.
Alisema JKT na Magereza wana nguvu kazi
kubwa wakiwamo wafungwa ambao hawahitaji
fedha yoyote kufanya kazi kwani ni wajibu wao,
na kwamba kila mkoa kuna magereza hivyo
askari waliopo katika magereza hayo wakafanye
kazi.
Alisema wafungwa waliofungwa katika
magereza wanapewa chakula kutoka katika
bajeti kuu, hivyo wanapaswa kufanya kazi.
Rais Magufuli alisema hata fedha anazotarajia
kuzipata kwa ajili ya utengenezaji wa madawati
mengine kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
na PPF anasita kuvipatia vyombo hivyo vya
ulinzi na usalama kwa kuogopa kuchukua muda
mrefu.
“Kama mmeshindwa mniruhusu niwa ‘involve’
wakuu wa mikoa, nina uhakika nikimwambia
Makonda akiwahusisha vijana wa vijiweni mwezi
mmoja madawati yataisha. Sasa mnisaidie ndugu
zangu makamanda mkatengeneze madawati.
Nimeona bora niongee hapa ili nisitoke na
kiungulia, ila nyie ndiyo mtoke na kiungulia,”
alisema Magufuli
Rais Magufuli alisema anahitaji madawati
haraka ili kuondoa uhaba unaozikabili shule za
sekondari na msingi wa madawati 1,400,000.
Alisema hadi sasa zaidi ya madawati 1,000,000
sawa na asilimia 88 ya madawati yaliyohitajika
kwa shule za msingi na asilimia 95.8 kwa shule
za sekondari yamepatikana.
Rais Magufuli alisema kwa sasa kwa shule za
msingi imebaki asilimia 11.2 kumaliza tatizo la
madawati, huku kwa shule za sekondari imebaki
asilimia 4.2,
Alisema tangu atoe agizo kwa wakuu wa wilaya
na mikoa ya kutengeneza madawati,
halmashauri 25 zimefikia malengo kwa upande
wa shule za msingi na halmashauri 46 kwa
shule za sekondari.
Katika mgawanyo wa madawati hayo, mkoa wa
Dar es Salaam ulipata madawati 5,370, mikoa
mingine na idadi yao katika mabano ni Pwani
(4,833), Morogoro (5,907), Lindi (4,295), Mtwara
(5,370), Ruvuma (4,833), Iringa (3,757), Njombe
(3,222), Mbeya (3,759), Songwe (3,222), Rukwa
(2,285), Katavi (2,683) Unguja (3,200), Pemba
(1,800) na Tanga (6,444).
Kadhalika, Rais Magufuli alisema baada ya
kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa
shule za msingi na sekondari, idadi ya
wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la
kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi
1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584
sawa na ongezeko la asilimia 84.5 hali
iliyosababisha upungufu wa madawati
1,400,000.

Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system