Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefanya uzinduzi wa ripoti ya haki za binadamu kibiashara ya mwaka 2015 ambayo imeonyesha jinsi hali ilivyo kwa sekta tatu ambazo walizifanyia utafiti za sekta ya habari, sekta ya usafirishaji wa abiria na mizigo na kutizama hali ilivyo kwa wabeba mizigo wa mlima Kilimanjaro.
Akizungumza kuhusu sekta ya habari, mgeni rasmi katika uzinduzi wa ripoti hiyo, Kaimu Mkurugenzi na Sera wa Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Alfred Mapunda alisema ripoti hiyo inawapa nafasi kama serikali kufahamu ni sekta zipi ambazo bado zinahitaji kufanyiwa kazi kutokana na mapungufu yaliyopo.
DSC_0326
Kaimu Mkurugenzi na Sera wa Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Alfred Mapunda akitoa hotuba katika uzinduzi wa ripoti ya haki za binadamu kibiashara ya mwaka 2015.
Alisema pamoja na kazi ambayo serikali imekuwa ikiifanya lakini kwa waandishi wa habari inabidi kufika hatua watambue haki zao za msingi kwa kuwabana mabosi zao ili waweze kuwa na mikataba ya kazi wanazofanya.
“Ripoti kwa upande wetu sisi inatupa mwanga wa kujua nini tunatakiwa kufanyia marejebisho maana kama imevyotolewa bado kuna maeneo yanaonekana kuwa na shida lakini tutakaa na kufanyia kazi,
“Kwa upande wa waandishi wa habari ripoti imeonyesha hali sio nzuri lakini niwambie jambo inabidi ifike hatua waandishi wajitambue na kujua mahitaji yao ni nini,” alisema Mapunda.
DSC_0318
Mtafiti wa ripoti, Clarence Kipobota akizungumza kuhusu ripoti hiyo.
Nae mtafiti wa ripoti hiyo, Clarence Kipobota alisema hali ya waandishi wa habari, madereva wa mabasi na magari ya mizigo pamoja na watu wanaotumiwa kubeba mizigo katika Mlima Kilimanjaro kutokuwa na mikataba sio athari kwao pekee kwani hata serikali inakosa mapato iliyotakiwa kuyapata,
“Serikali inahitaji kukusanya kodi ili kuwa na fedha za kuleta maendeleo lakini kama hakuna mikataba inamaana serikali inakosa kodi yake na hata wafanyakazi wenyewe kuna fursa wanazikosa kwa kukosa mikataba,” alisema Kipobota.
DSC_0300
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba akitoa ushauri kwa serikali.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema ni vyema sheria za nchi zikasimamiwa kama inavyostahili ili kumaliza changamoto ambazo zimekuwa zikijitokea kwa sasa kama jinsi ripoti hiyo ambavyo imeonyesha.
Aliongeza kuwa mbali na vipaumbele vikubwa ambavyo walivifanyia kazi lakini pia kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki za wanawake na watoto katika maeneo ambayo walifika kufanya utafiti na hivyo kupitia ripoti hiyo ni wasaa sasa wa serikali kufanyia kazi changamoto hizo.
DSC_0336
Kaimu Mkurugenzi na Sera wa Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Alfred Mapunda akikata utepe kuashirikia ufunguzi wa ripoti.