Comments


NEC YAANZA MAANDALII YA UCHAGUZI 2020

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaendelea na maandalizi ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa kuboresha daftari la wapiga kura ili kuweka taarifa za walengwa wakiwemo watakaopiga kura baada ya kufikisha umri wa kupiga kura.

Aidha, itawahusu walioshindwa kupiga kura katika chaguzi zilizopita kutokana na sababu mbalimbali. Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Ofisa Uchaguzi wa Tume hiyo, Adam Nyando wakati akikabidhi taarifa za Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa mkoa wa Pwani.

Alisema, baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka 2015, wameanza maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao na si kwamba kwa sasa Tume imelala.

“Watu wanafikiri uchaguzi ukishaisha ndio kazi imekwisha kumalizika kwa uchaguzi mmoja ni maandalizi ya uchaguzi ujao kwani kwa sasa tunaendelea na uboreshaji wa daftari la wapigakura pamoja na kura za maoni,” alisema Nyando.

Alisema uchaguzi uliopita ulikwenda vizuri na hakukuwa na matatizo makubwa licha ya matumizi ya mfumo mpya wa BVR, lakini matokeo yake umekuwa mfumo mzuri na umepata mafanikio makubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, akizungumza alitumia fursa hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kufanya uchaguzi mzuri usiokuwa na vurugu wala uvunjifu wa amani.

Ndikilo alisema nchi nyingine kipindi cha uchaguzi ni kipindi kibaya cha uvunjifu wa amani, ikiwa ni pamoja na umwagikaji mkubwa wa damu, hasa kwa pande zisizokubaliana matokeo.

“Uchaguzi ulienda vizuri licha ya changamoto zilizojitokeza za hapa na pale lakini watu walivumiliana na kukubaliana na matokeo kilichobaki sasa ni kufanya kazi ili kuwaletea maendeleo wananchi, kikubwa ni tume kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na usafiri na ucheleweshwaji wa matokeo kwa baadhi ya sehemu,” alisema Ndikilo.

Akikabidhi taarifa hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ofisa Uchaguzi wa mkoa, Shangwe Twamala alisema mkoa huo umepata nakala 47 ambazo zitasambazwa kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi. 

Alisema taarifa hizo zitasambazwa kwenye ofisi za mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za miji na wilaya na taasisi za elimu ya juu.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system