Comments


FAINI KUONGEZWA KWA MAGARI YATAKAYOZIDISHA UZITO

Serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza faini inayotozwa hivi sasa kwa magari yanayozidisha uzito, ili kulinda miundombinu ya barabara za lami zinazogharimu fedha nyingi za umma ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Hayo yamesemwa na naibu wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwini Ngonyani, muda mfupi kabla ya kukagua kituo cha mzani cha Itigi wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Alisema kuwa lengo la serikali kuweka vituo vya mizani barabararani, sio kukusanya ushuru kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiri, madhumuni ni kutoa adhabu ya kulipa faini kwa madereva wanaozidisha uzito kinyume na sheria.

Alisema kuwa madereva wachache wenye utamaduni wa kuzidisha uzito, wasipodhibitiwa, miundombinu ya barabara haitachukua muda mrefu itaharibika na lawama itaelekezwa kwa serikali kwamba inajenga barabara chini ya kiwango.

“Ili kukomesha kabisa tabia hii ya baadhi ya madereva kuzidisha uzito kwenye magari yao, upo umuhimu adhabu ya faini kwa makosa hayo,ili tuweze kulinda barabara zetu ambazo ni muhimu kwa uchumi wa nchi,” alifafanua.

Katika hatua nyingine, Waziri Ngonyani, ameziagiza serikali za mitaa nchini, kuwachukulia hatua kali wote wanaoharibu barabara zikiwemo za lami.

“Barabara yenye urefu wa kilometa 89.3 inayoanzia Manyoni mjini kwenda Chaya mpakani mwa mkoa wa Tabora, imekamilka hivi karibuni kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini kwa makusudi, baadhi ya wananchi, wameanza kuiharibu,” alisema.

Ngonyani alisema barabara hiyo iliyogharimu zaidi ya shilingi 113.5 bilioni, serikali haiwezi kuwavumilia wananchi hao wachache wenye lengo la kurudisha nyuma maendeleo.

“Ni wajibu wa serikali za mitaa kwenye maeneo husika, kutoa adhabu kali kwa waharibifu wote wa miundombinu ya barabara, zikiwemo alama za barabarani,” alisema.

Akifafanua zaidi, Ngonyani alisema kwa mujibu wa taarifa ya meneja TANROADS mkoa wa Singida, mhandisi Kapongo, wapo baadhi ya wananchi wanachimba pembezoni mwa barabara, ili waweze kuiba kokoto, kufuta alama za barabarani na nondo, hawa wakinaswa, wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwao na kuogofya wengine.

“Hatuwezi kuvumilia tabia hii iendelee … serikali ya awamu ya tano imeishasema kuwa itakuwa ni ya viwanda, ustawi wa viwanda utapatikanaje kama watu na akili zao wanaharibu kwa makusudi miundo mbinu ya barabara,” alisema.

Wakati huo huo, naibu waziri huyo, ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa madiwani kushirikiana na uongozi wa halmashauri zao kupata mwarobaini wa tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system