SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeendesha msako wa kushtukiza wa nguo za ndani za mitumba katika masoko yaliyoko Manzese na Karume jijini Dar es Salaam na kukamata magunia 20 ya nguo hizo za thamani ya Sh milioni tisa, zilizokuwa zikiendelea kuuzwa licha ya kupigwa marufuku.
Akizungumza muda mfupi baada ya kukamata nguo hizo juzi, Ofisa Viwango wa shirika hilo, Johnson Kiwia, alisema mitumba hiyo ilizuiwa kuuzwa katika soko la ndani kwa kuwa haikidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa, hivyo kutofaa kutumiwa na binadamu.
Alisema, wamefanya ukaguzi wa kushtukiza wilayani Ilala kwenye Soko la Karume na Kinondoni katika Soko la Manzese na kuona jinsi wateja wanavyozikimbilia nguo hizo licha ya kuelezwa madhara yake.
Kiwia alisema nguo hizo zilizokamatwa zitateketezwa na kwa mujibu wa Sheria ya Viwango vya Ubora namba 9 ya mwaka 2009, uteketezaji hufanywa kwa gharama za mmiliki wa bidhaa isiyo na ubora.
Alisema pia kuwa, mmiliki huweza kushtakiwa mahakamani na kufungwa au kutozwa faini ya kuanzia Sh milioni 50 hadi Sh milioni 100 au vyote viwili.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa TBS, Baptister Bitaho, alisema mfanyabiashara anayekiuka Sheria ya Viwango kwa kuingiza, kuzalisha au kusambaza bidhaa zisizo na ubora huweza kuamriwa kuzirejesha zilikotoka na ikibidi kufungiwa biashara.
0 comments:
Post a Comment