WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa saa 48 kwa Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuwa amewaondoa kazini watumishi 89 wanaofanya kazi katika halmashauri hiyo kwa Mikataba.
Aliyasema hayo alipozungumza na watumishi na watendaji wa manispaa hiyo, huku akiweka bayana kwamba halmashauri hiyo inaongoza kwa kuwa na watumishi wa Mikataba, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za utumishi.
Akiendelea na mkutano huo, ghafla Waziri Mkuu alimsimamisha Kaimu Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Zaituni Hassan na kumuuliza idadi ya watumishi wa Mikataba katika halmashauri hiyo ambapo ofisa huyo alijibu kuwepo kwa watumishi 89.
Jibu hilo lilimfanya Waziri Mkuu kuhoji sababu ya kuwepo kwa idadi kubwa hiyo na kujibiwa kuwa hatua hiyo ilitokana na wengi wao kukosa sifa za kuajiriwa huku akisema wengi wao ni madereva.
Majaliwa alieleza kuwa wanaotakiwa kuajiriwa kwa Mikataba ni walimu wa Masomo ya Sayansi na watendaji wa mitaa hivyo kama madereva hao hawana sifa ni vyema wakaondolewa kwa vile wanaziba nafasi za watu wenye sifa za kuajiriwa.
Alisema kutokuajiriwa ni moja ya sababu za kuwepo watumishi hewa hivyo alisema hadi kufikia Julai 30, mwaka huu, Ofisa Utumishi huyo awe amejiridhisha kuhusiana na sifa za watumishi hao ili wasio na sifa waondolewe na wenye sifa waajiriwe huku akisema zoezi hilo lifanyike katika idara zote.
0 comments:
Post a Comment