Comments


Hoseah: Chagueni viongozi kwa hoja


MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Dk Edward Hoseah amewatahadharisha wananchi kuwachagua viongozi bora na waadilifu ambao wana ushawishi wa hoja na sio ushawishi wa fedha.
Dk Hoseah aliyasema hayo juzi usiku katika kipindi cha ‘Mtiti wa Uchaguzi’ kinachorushwa hewani na kituo cha Televisheni cha ITV, ambapo alizungumzia mambo mbalimbali yakiwemo rushwa na maadili wakati wa uchaguzi.
Akizungumzia hilo, Dk Hoseah alisema Sheria ya Gharama za Uchaguzi inaeleza bayana kuhusu matumizi ya fedha katika kampeni za uchaguzi kwa vyama na wagombea na imeweka ukomo kwa fedha hizo.
“Niwatahadharishe wapiga kura, chagueni viongozi waadilifu, msichague viongozi wenye ushawishi wa fedha, bali chagueni wenye ushawishi wa hoja kwa sababu ndio viongozi bora,” alisema Dk Hoseah.
Alisema pamoja na sheria hiyo kuainisha kiasi cha fedha kinachotakiwa kutumika na wagombea wa nafasi mbalimbali, lakini pia sheria hiyo inakataza ushawishi wa fedha kama njia ya kuwapata wapiga kura.
Akifafanua Dk Hoseah alisema Sheria ya Gharama za Uchaguzi inaruhusu wagombea kutoa fedha kwa timu yake ya kampeni ili kuwafikia wapiga kura kunadi sera zake, na kwamba inakataza mgombea kutoa fedha kwa ajili ya kununua vyakula,vinywaji au kuwapa wapiga kura nauli.
Akizungumzia uelewa wa wananchi kuhusu sheria hizo na elimu ya uraia pamoja na masuala ya rushwa na uchaguzi, alisema bado kuna changamoto kubwa kwa serikali kuhusu kusambaza elimu ya uraia kwa wananchi.
“Niweke wazi tu kwamba bado wananchi wengi hawana elimu ya uraia , niiombe serikali kutenga fedha za kutosha ili elimu iwafikie wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini,” alisema Dk Hoseah.
Akizungumzia makali ya Takukuru, Dk Hoseah alisema ni vyema serikali ikaangalia upya jinsi ya kuunganisha kazi ya uchunguzi na ile na mashtaka ili iwe pamoja na wao wapewe meno ya kusimamia hayo.
“Tuna mawakili 175, sasa ukiwaacha tu bila kutumika wataacha kazi wataenda kwingine, ni vyema tupewe meno tuwashughulikie watuhumiwa wa rushwa na tuombe vyombo husika, viunganishe Sheria ya Rushwa na ile ya Uhujumu Uchumi iwe moja,” alisema Dk Hoseah.

Alisema kama sheria hizo mbili zitaunganishwa itakuwa sheria moja yenye nguvu, ambayo watuhumiwa wa makosa hayo wataiogopa kwa kuwa adhabu zake ni kubwa kulingana na makosa, lakini ikiwa sheria ya rushwa itaendelea kuachwa yenyewe,wala rushwa hawaiogopi.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system