Nahodha John Bocco 'Adebayor'
Mabao mawili ya nahodha John Bocco 'Adebayor' na mengine mawili ya washambuliaji wa kimataifa Didier Kavumbagu na Kipre Tchetche yalitosha kuipa Azam FC ushindi wa 4-2 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana.
Matokeo ya mechi hiyo ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu Tanzania Bara
iliyochezeshwa na Mwamuzi Bora wa msimu uliopita, Israel Nkongo,
yameifanya Azam kufikisha pointi 22, hivyo kuing'oa Yanga kileleni mwa
msimamo kwa mara ya kwanza baada ya siku 47 (saa 1128) tangu Septemba 13
timu hiyo ya Jangwani ilipouanza msimu kwa kushinda 2-0 dhidi ya
Coastal Union.
Kavumbagu aliyekuwa katika ubora wake jana akipika mabao mawili,
alifungua karamu ya mabao ya Azam jana akimalizia kiufundi krosi ya beki
wa kulia Shomari Kapombe dakika ya nne ya mchezo kabla ya Bocco kufunga
la pili dakika mbili baadaye.
Dakika moja baada ya nusu saa ya mchezo, Najim Magulu aliwafungia
wenyeji akimalizia mpira uliowababatiza mabeki wa Azam baada ya faulo
kali iliyopigwa na mshambuliaji Saad Kipanga na kuzifanya timu hizo
kwenda mapumzikoni matokeo yakiwa 1-2.
Bocco alifunga bao la tatu kwa penalti iliyoamuliwa na refa Nkongo
baada ya Kapombe kukwatuliwa na Paul Mhidze ndani ya boski dakika ya 64,
lakini dakika tano baadaye Emmanuel Pius akajibu mapigo kwa kuipatia
JKT Ruvu goli la pili.
Baada ya bao hilo, Kocha wa Azam FC alifanya mabadiliko kwa
kuwaingiza Erasto Nyoni kwa ajili ya kuongeza ulinzi na Tchetche ili
kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji, mabadiliko ambayo yalijibu
baada ya Muivory Coast huyo kufunga bao la nne akikokota mpira hadi
ndani ya boksi kabla ya kupiga shuti kali lililompita kipa Shaban
Dihile.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo jana, Tanzania Prisons
walishinda 1-0 nyumbani dhidi ya African Sports ya Tanga kwenye Uwanja
wa Sokoine jijini Mbeya, shukrani kwa bao la tuta lililopigwa na
'muuaji' wa Simba, Mohamed Mkopi na kuiwezesha timu yake kupanda hadi
nafasi ya sita.
0 comments:
Post a Comment