MBUNGE mteule wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM) amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia mbio za kuwania Spika wa Bunge hadi chama chake kitakapotoa utaratibu.
Amesema pamoja na baadhi ya makada wenzake wa CCM kuanza kujipitisha kuwania nafasi hiyo kwake anaamini CCM ndicho kitatoa utaratibu wa kupatikana spika.
Zungu alitoa kauli hiyol Dar es Salaam jana alipozungumza na wanahabari baada ya jina la mwanasiasa huyo kutajwa katika kuwania uspika wa Bunge.
Alisema yeye hajawahi kutamka kuwania nafasi hiyo zaidi ya wabaya wake wa siasa kutumia jina lake kwa malengo wanayojua wao.
“Mimi bado sijatamka kwa kinywa changu kama ninataka kuwania uspika ila utaratibu wa jambo hili utatolewa na chama.
“Hivyo kama mnataka kujua nitawania ama laa subiri kwanza chama kitoe utaratibu ndipo nitakuwa na la kusema lakini kwa sasa hapana.
“CCM ni chama tawala kina utaratibu wake nitakuwa mtu wa ajabu kusema nitawania kuwa Spika wa Bunge wakati hata chama hakijatoa utaratibu,” alisema Zungu.
Hata hivyo, alisema anajivunia namna bora anavyotekeleza ilani ya CCM kwa wapiga kura wake wa Ilala.
Alisema kila mara wamekuwa msaada mkubwa kwake na wameendelea kumuamini kwa kumchagua tena.
Zungu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge katika Bunge la 10 ni miongoni mwa wenyeviti wanaosifika kwa rekodi ya kuendesha vizuri Bunge.
Anatajwa kama kiongozi anayepewa nafasi kubwa ya kuteuliwa na chama chake cha CCM kuwania nafasi hiyo ya Spika wa Bunge ikiwa ataridhia kufanya hivyo.
Baadhi ya wabunge wa CCM na hata vyama vya upinzani wamekuwa wakimtaja mbunge huyo wa Ilala kama ni moja ya nguzo ya Bunge na hana upendeleo.
0 comments:
Post a Comment