Comments


USAFI UPEWE KIPAUMBELE RC IRINGA.....................................................


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza.


MKUU wa Mkoa Iringa, Amina Masenza ametoa mwito kwa wananchi mkoani humu kuufanya usafi wa mazingira kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku ili kuepuka magonjwa ya milipuko, ikiwemo kipindupindu na kuhara.
Aidha, amesema maisha bora yatakuwa ndoto ya mchana endapo wananchi wenyewe hawatajitoa kuhakikisha wanauthamini usafi wa mazingira yao hasa kwa kujenga vyoo bora na kuvitunza, kusafisha maeneo yote yanayowazunguka na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni angalau kwa vipindi vitano kwa siku.
Masenza aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa wiki ya usafi wa mazingira kimkoa uliofanyika katika kijiji cha Uhambingeto wilayani Kilolo mkoani hapo.
 Maadhimisho hayo ya wiki ya usafi wa mazingira yanahusisha unawaji mikono.
Kimataifa huwa kuna siku ya maadhimisho ya kunawa mikono pamoja na siku ya choo. Nchini yalianza kuadhimishwa mwaka juzi. Kwa mujibu wa Masenza, endapo wananchi wataendelea kutupa taka hovyo huku huduma ya usafi katika mkoa huu ikiendelea kuwa duni, hakuna mafanikio yatakayofikiwa katika vita dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
Alisema, “Ni wajibu wa kila mmoja kushiriki usafi binafsi na wa mazingira yanayo mzunguka ikiwemo vyoo, kuhakikisha hayawi chanzo cha maradhi ya kuhara na kipindupindu”. Kwa maelezo yake, suala la kunawa mikono nalo ni la muhimu na linapaswa kupewa kipaumbele zaidi, hata kama wananchi watajitoa ipasavyo kushiriki usafi wa vyoo na mazingira mengine yanayowazunguka.
“Mkijenga vyoo bora mvitumie”, Masenza aliwaeleza wananchi katika uzinduzi huo na kuongeza kuwa kuna haja ya kuhamasishana kuhusu matumizi ya vyoo bora kwa sababu wapo wanaovijenga na kutovitumia.
Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zimeeleza kuwa ugonjwa wa kuhara unaotokana na uchafu wa mazingira ni miongoni mwa magonjwa matano yanayosababisha vifo vya watoto wengi wenye umri chini ya miaka mitano Tanzania, hivyo kuhitaji jitihada kuukomesha.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system