WATOTO wawili wamekufa papo hapo na watu wengine 53 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wanasafiria kuacha njia na kupinduka kijiji cha Pida, wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philipo Kalangi alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa saba mchana katika eneo la Kijiji cha Pida, Wilaya ya Butiama.
Kamanda Kalangi alilitaja basi lililopata ajali hiyo kuwa ni la Kampuni ya Batco yenye namba za usajili T. 867 DAK, iliyokuwa inaendeshwa na Busunga Peleka (35) mkazi wa Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, na kwamba ilikuwa ikitokea Sirari wilayani Tarime kwenda jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi mkoani Mara, majeruhi wa ajali hiyo ni 20 na wengi wamelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda na wawili wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa mjini Musoma.
Hata hivyo, gazeti hili lilipofuatilia katika Hospitali Teule (DDH) Bunda ambako majeruhi wengi wamelazwa, Kaimu Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo, Suzana Sangaro alisema majeruhi wote waliopokelewa kulazwa hapo ni 53.
Kaimu muuguzi mkuu huyo alisema majeruhi wa kiume ni 31 na wa kike ni 22, ambapo kati yao watoto wa kike ni wawili na wa kiume wawili. Alisema kuwa majeruhi kati ya majeruhi hao wanne wana hali mbaya sana na wawili kati yao wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza.
Kamanda Kalangi alisema dereva wa basi hiyo baada ya ajali hiyo kutokea alitoroka, lakini baadaye alijisalimisha polisi na anashikiliwa na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu zote za kipolisi kukamilika.
0 comments:
Post a Comment