Nyota wa Tanzania na timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Samatta amefunga goli moja kwenye ushindi wa magoli 2-0 iliyoupata timu yake ya TP Mazembe kwenye mchezo wa marudiano wa fainali ya vilabu bingwa Afrika dhidi ya USM Alger mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Stade TP Mazembe Lubumbashi, Congo DR.
Ushindi huo umeifanya TP Mazembe ichukue kombe la vilabu bingwa barani Afrika kwa mara ya tano lakini ikiwa ni mara ya kwanza kwa wachezaji wa kimataifa wa Tanzania wanaokipiga kwenye klab hiyo Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Samatta na Ulimwengu wameweka rekodi ya kuwa watanzania wa kwanza kunyanyua kombe la klabu bingwa barani Afrika huku nyota wengine waliong’ara zamani kwenye medani ya soka wakishindwa kufanya hivyo.
Mazembe ilishachukua kombe hilo mwaka 1967, 1968, 2009, 2010 na mwaka huu 2015 imefanya hivyo.
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo hakikua na mashambulizi mengi kwa timu zote mbili hasa kwa upande wa TP Mazembe ambao walionekana kama wanalinda ushindi wao walioupata kwenye mechi ya awali nchini Algeria. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Kipindi cha pili Mazembe walianza kusaka ushindi na wakafanikiwa kupata goli la kuongonza lililofungwa na Mbwana Samatta kwa mkwaju wa penati dakika ya 75 baada ya Roger Assale kuangushwa na beki wa USM Alger akiwa kwenye eneo la hatari.
Goli hilo limemfanya Samatta kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo kwa kufikisha jumla ya magoli nane na kumpiku Bakry ‘Al Medina’ Babiker wa Al Merreikh ambaye wamekua wakichuana kwa muda mrefu.
Wakati dakika zikiwa zinaelekea ukingoni Mbwana Samatta alitengeneza goli jingine ambalo lilifungwa na Roger Assale ambalo lilimaliza kabisa ndoto za USM Alger kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza.
TP Mazembe wamekuwa mabingwa kwa jumla ya magoli 4-1 dhidi ya USM Alger, mchezo wa fainali ya kwanza uliochezwa Algiers, Algeria ulimalizika kwa Mazembe kushinda kwa magoli 2-1 huku mchezo wa marudiano ambao umepigwa jijini Lubumbashi, Congo DR ukimalizika kwa TP Mazembe kushinda kwa magoli 2-0.
Ubingwa huo unawapa Mazembe tiketi ya kushiriki fainali za vilabu bingwa duniani zitakazofanyika December mwaka huu nchini Japan.
TP Mazembe inaungana na mabingwa wa Ulaya Barcelona na mabingwa wa Copa Libertadores River Plate ambao tayari wamejihakikishia nafasi kwenye fainali hizo huku mabingwa wa Oceania klabu ya Auckland City pamoja na mabingwa wa Amerika Kusini Club America wakiwa tarari kwenye orodha hiyo.
Bingwa wa Asia kati ya Al-Ahli au Guangzhou Evergrande Taobao na J-League wataungana wataungana na vilabu vingine na kufanya jumla ya vilabu nane vitakavyocuana kwenye fainali hizo.
0 comments:
Post a Comment