ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuungwa mkono na umoja wa vyama vingine vitatu, Edward Lowassa, amewataka wafuasi na wanachama wa vyama hivyo kuendelea kuwa watulivu baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu.
Lowassa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa vyama hivyo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuwa wao bado wanaendelea kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzamnia Ibara ya 41(7), “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa Ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”
Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya zabuni ya kufua umeme ya Kampuni ya Richmond, alisema wananchi waendelee kuwa watulivu na Ukawa itaendeleza harakati za kisiasa katika nyanja mbalimbali za kidemokrasia ili kutekeleza azma ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Aidha, Lowassa alisema Ukawa itaendelea kudai Katiba ya wananchi itakayohakikisha kuwa Tanzania inakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na serikali inayowajibika kwa umma. Akizungumzia juu ya ushiriki wa wabunge wa Ukawa katika ufunguzi wa Bunge la 11 mjini Dodoma ambalo litahutubiwa na Rais John Magufuli wiki hii, alisema siku hiyo ikifika ndio itajulikana nini kitafanyika.
“Sisi hatuna tatizo na Serikali wala Bunge hivyo hilo la ufunguzi wa Bunge tusubiri tutalijua siku hiyo hiyo,” alisema Lowassa aliyeperusha bendera ya Chadema kupitia Ukawa na kushika nafasi ya pili nyuma ya Dk Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyeshinda kwa asilimia 58.46 ya kura halali.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa Ukawa wamelaani mauaji ya kikatili ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita na aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Busanda, Alphonce Mawaz0
0 comments:
Post a Comment