Comments


MAKAMU WA RAIS AWAASA VIJANA WA KIISLAM KUZINGATIA MISINGI YA DINI




Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewaasa  vijana wa Kiislam nchini kuzingatia misingi waliyoipata ya elimu ya Kur-an na elimu ya dunia kupambana na matatizo mbalimbali yanayolikwaza Taifa yakiwemo ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya, ujambazi na mengineyo.

Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jana katika hafla ya kuwapongeza vijana wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tanzania waliohitimu katika vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency, Jijini Dar es salaam,

Samia alisema anaamini kwamba misingi hiyo itawapa miongozo ya kupambana na matatizo hayo na hivyo kumwezesha kijana kuwa kioo cha jamii yeyote ile atakayoishi na kufanya nayo kazi.

Makamu wa Rais aliwaasa pia vijana hao waliohifadhi Kur-an na wasomi kutenda matendo mema katika maisha yao kwa kuwa elimu waliyoipata ni daraja na heshima waliyonayo kwa Mungu na hapa Duniani.

“Heshima mliyopata ya kuwa mabingwa wa elimu ya Kur-an na elimu ya sayansi ya dunia, iwape muongozo katika maisha yenu,” alisema Samia na kuongeza “Kile mlichobeba, ujumbe mzuri na mzito uliomo kwenye Kur-an mkioneshe kwa vitendo, na pia vitendo vyenu vitoe tafsiri/taswira ya kuonesha nyinyi ni nani.”

Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuipongeza Jumuiya hiyo chini ya uenyekiti wa Sheikh Othman Kaporo kwa kuanzisha mpango huo madhubuti zaidi ya miaka 30 iliyopita wa kuwalea vijana kiimani na kuwaendeleza kielimu, ili hatimaye walinufaishe Taifa lao.

Mapema, akizungumza katika hafla hiyo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliwaomba Mabalozi wa nchi za Kiarabu nchini kuangalia uwezekano  wa kuanzisha shule itakayofundisha lugha ya kiarabu.

Alisema Waislamu wengi wanasoma Kur-an lakini hawajui kile wanachosoma kwa sababu ya kutokujua lugha ya Kiarabu ambayo ndiyo lugha ya Kur-an.

“Wengi tunasoma Kur-an, lakini hatujui kwa sababu hatujui Kiarabu ambayo ndiyo lugha ya Kur-an. Ni wajibu wa serikali kufundisha Kiarabu…. Lakini mjue nchi yetu haina dini, watu wake wana dini; sasa Mabalozi, nchi zenu za Kiislam zina wajibu wa kufundisha wenzenu Kiarabu,” alisema Alhaji Mwinyi na kuongeza

“Ndugu zetu mtufunze Kiarabu, mtufungulie skuli ya kusomesha lugha ya Kiarabu. Waingereza wanayo inaitwa British Council, wanafundisha lugha ya Kiingereza; jambo hili mlifikirie, lugha ya Kiarabu ni lugha ya Kur-an.”

Katika hafla hiyo, pamoja na kuonesha video ya safari ya Kur-an nchini Makamu wa Rais alitoa vyeti kwa vijana wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Kur-an Tanzania wapatao 20 waliohitimu katika vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi. 
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment

Disqus Shortname

Comments System

Disqus Shortname

Comments system