Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya juu kote nchini wametakiwa kutumia muda mwingi kujisomea na kuepuka kujiingiza kwenye vitendo vya vurugu , migomo na maandamano yasiyo na tija kwa taifa ambayo yamekuwa yakiwapunguzia ufanisi katika masomo yao.
Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda wakati akizungumza na Jumuiya ya wanataaluma wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) kwenye kongamano la 3 lililowakutanisha wahitimu wa chuo hicho mwaka huu, wanataaluma waliopo na wale waliowahi kusoma katika chuo hicho (CBE Alumni Association) na wadau mbalimbali jijini Dar es salaam.
Akiwa mgeni rasmi katika kongamano hilo na mmoja wa wahitimu wa siku nyingi wa chuo hicho Kamanda Suzan Kaganda amesema wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya juu wanapaswa kutambua kuwa elimu wanayoipata katika vyuo hivyo sio kwa ajili ya manufaa yao binafsi bali ni kwa manufaa ya taifa zima hivyo wanatakiwa kuwa makini na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
“Naomba nisisitize kuwa elimu mliyoipata na mnayoendelea kuipata chuoni hapa sio kwa ajili ya manufaa yenu binafsi bali ni kwa ajili ya manufaa ya taifa, wakati mwingine mnapoteza muda mwingi pindi mnapojiingiza kwenye migomo na maandamano barabarani kushindana na Serikali, muda ambao mgeutumia kujisomea ninyi wenyewe” Amesisitiza Kamanda Suzan.
Amewataka wahitimu na wanafunzi wa chuo hicho kutumia elimu na ujuzi walioupata kusaidia katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali ya awamu ya tano kwa kuhakikisha wanazitumia vizuri fursa za ajira zilizopo kujiajiri na kuajiri wengine.
“Taifa letu linazo fursa nyingi, kinachotakiwa ni wazawa kuazisha makampuni yatakayoweza kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo zitauzwa duniani na hatimaye kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesisitiza.
Aidha, amekipongeza chuo cha CBE kwa kupiga hatua na kupata mafanikio makubwa katika utoaji wa elimu tangu kuanzishwa kwake miaka 51 iliyopita kwa kuwa maendeleo makubwa kwa taifa lolote hayawezi kupatikana bila kuwaelimisha wake katika biashara na Ujasiriamali elimu inayotafsiri uchumi wa viwanda pia.
“Nachukua fursa hii kuupongeza uongozi wa CBE kwa kuongeza matawi ya chuo katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka pamoja na fani katika ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, Shahada za Uzamili na Uzamivu” Amesema Suzan Kaganda.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha CBE, Prof. Emanuel Mjema akizungumza wakati wa kongamano hilo amesema kuwa chuo anachokiongoza kimeendedelea kupata sifa ya kuwa chuo bora ndani na nje ya nchi kwa kuwa kimewatoa viongozi mahiri ambao waliotoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Ameeleza kuwa CBE kilianzishwa mwaka 1965 kikiwa na wanafunzi 20 tu ili hali sasa kina wanafunzi zaidi ya 11,000 huku fani za elimu zikiongezeka kutoka ngazi ya cheti hadi shahada za Uzamili na masomo ya Uzamivu ambayo yanatolewa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mashariki cha Finland.
“ Chuo chetu kimepiga hatua kubwa kimaendeleo toka kilipoanzishwa mwaka 1965, kimepata mabadiliko makubwa tumekuwa kitaaluma, kimachapisho na pia kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo fursa za biashara wakati huu ambao Serikali inahamia mkoani Dodoma,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa chuo hicho kitaendelea kusimamia weledi katika utoaji wa elimu hapa nchini ili kiendelee kutoa vijana wenye weledi na uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali kulingana na fani walizosomea.
“Chuo chetu tunasisitiza ubora wa elimu, tunafanya mchujo kwa kila mwaka ili kudhibiti ubora wa elimu yetu wale wasiofikia viwango kwa kila mwaka tunawaacha warudishwe nyuma sio kila anayeingia hapa lazima ahitimu masomo yake wale wasiokidhi viwango na kuendana na kasi ya masomo chuoni hapa wanajiondoa wenyewe,” amesisitiza Prof. Mjema.
Katika hatua nyingine Prof. Mjema amebainisha kuwa Novemba 12 Chuo hicho kitaadhimisha mahafali ya 51 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment