Tukio hilo lilitokea jana saa sita mchana katika eneo la Hamugembe, Manispaa ya Bukoba mjini.
Kabla ya waandishi hao kufukuzwa, walikwenda kuwaona waathirika hao ili kujua jinsi agizo la Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, lilivyotekelezwa baada ya kumwagiza Mkurugenzi wa Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya, apeleke msaada wa mahema kwa waathirika wa Hamugembe.
Kutokana na agizo hilo, jana waandishi wa habari walifika katika kata hiyo kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo, lakini walinusurika kupigwa.
Miongoni mwa walionusurika ni pamoja na Mwandishi wa Habari wa MTANZANIA, Editha Karlo na Audax Mtiganzi wa ITV.
Katika tukio hilo, waathirika hao walisema hawataki kuhojiwa kwa kuwa hawaoni faida ya mahojiano kwani Serikali haiwasaidii chochote.
"Tumechoshwa na mahojiano ya kila siku kwa sababu hata mkiandika na kutangaza, Serikali haichukui hatua.
“Kuna waandishi wenzenu wa televisheni walikuja hapa wakaniambia nipange vitu na wakanipiga picha, lakini sijaona msaada wowote hadi leo kutoka serikalini.
“Huu ni udhalilishaji mnaotufanyia, mkitaka habari muwe mnakuja usiku kuangalia mazingira tunayolala, hatutaki kabisa kuwaona hapa.
“Sisi tunapata shida, hatuna mahema, hatuna chakula lakini nyinyi mnakuja kutuhoji, acheni kutuchezea,” alisema mmoja wa waathirika hao.
Alisema kila siku wanaona viongozi mbalimbali wakienda kutembelea lakini misaada haionekani, mtu unapewa msaada wa biskuti au kilo nane za mchele, huo ni msaada gani,” alifoka mwananchi huyo huku akichukua fimbo na kuwafukuza waandishi hao.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Hamugembe, Sudi Zuberi, alisema anaendelea kufuatilia misaada na itakapopatikana ataigawa kwa waathirika hao.
0 comments:
Post a Comment