Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hall of Fame Boxing Promotions Jay Msangi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusiana na pambano la bondia Ibrahim Class ambaye atapambana na bondia Jason Bedeman wa Afrika Kusini kuwania mkanda wa Light wa uzito wa Chama Cha WBF na Abdallah Pazi (Dulla Mbabe) ambaye atapambana na bondia , Zheng Chengbo wa China katika pambano la kimataifa.
Bondia Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ (kulia) akizungumza katika mkutano huo. Pazi atapambana na bondia Zheng Chengbo wa China katika pambano la kimataifa la uzito wa Super Middle. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Hall of Fame Boxing and Promotions, Jay Msangi
Bondia Ibrahim Class (kulia) akizungumza katika mkutano huo. Class atapambana na bondia Jason Bedeman wa Afrika Kusini kuwania mkanda wa Light wa uzito wa Chama Cha WBF. Kushoto ni bondia Abdallah Pazi
Bondia nyota nchini, Abdallah “Dulla Mbabe” Pazi atapanda jukwaani Oktoba 28 kupambana na bondia kutoka China, Zheng Chengbo katika pambano la kimataifa uzito wa Super Middle.
Mbali ya Mbabe, bondia mwingine wa Tanzania, Ibrahim Class ambaye ni bingwa wa kimataifa wa World Professional Boxing Federation (WPBF) na Universal Boxing Organization (UBO) naye atapanda ulingoni kuwania ubingwa wa kimataifa wa WBF kwa kupambana na bondia kutoka Afrika Kusini Bedeman ambaye ni bingwa wa zamani wa uzito wa light wa vyama vya WBA na IBO.
Akizungumza jijini jana, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hall of Fame Boxing Promotions Jay Msangi alisema kuwa mapambano hayo yatafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee hall na mabondia hao watawasili nchini wiki moja kabla ya pambano.
Msangi alisema kuwa maandalizi ya mapambano hayo yamekamilika na mabondia wote walikuwa kwenye maandalizi makali chini ya makocha wao.
Alisema kuwa Mbabe kwa sasa anasimamiwa na kocha wake, Shomari Kimbau wakati Class yupo chini ya kocha nyota nchini, Habib Kinyogoli na bingwa wa zamani wa Dunia, Rashid Matumla.
“Maandalizi yapo vizuri na mabondia wote wapi katika morali ya juu, Mbabe anataka kudhihirisha ubora wake nchini katika uzito wa Super Middle kwa kumchapa Mchina ambaye kwa sasa yupo katika timu ya Olimpiki ya China na ni moto wa kuotea mbali,”
“Class baada ya kumchapa Cosmass Cheka na kutwaa ubingwa wa UBO mwaka huu na kuchmapa Mzambia Mwasa Kabinga kwa TKO raundi ya tisa, sasa anataka kuonyesha kuwa ni nyota mpya ya ngumi za kulipwa nchini kwa kumchapa bondia huyo wa Afrika Kusini,” alisema Msangi.
Kwa upande wake, Mbabe alisema kuwa amejiandaa vizuri na anasubiri siku ya pambano lenyewe ili kuwapa raha Watanzania.
“Namsubiri Mchina kwa hamu sana, hatofika raundi ya tatu, sitataka adumu jukwaani kwa zaidi ya dakika 15,, nataka kumpa kipigo cha kihistoria ili aende kuwaambia wenzake kuwa kuna bondia hatari sana na wa kuogopwa hapa nchini,” alisema Mbabe.
Class alisema kuwa hana shaka na pambano na ushindi ni jadi yake. “Nipo fiti kwa ajili ya pambano, nipo tayari kwa changamoto, najua naye anajiandaa kama mimi, sitawaangusha Watanzania siku hiyo,” alisema Class.
0 comments:
Post a Comment