Sumaye alikuwa waziri mkuu wa Tanzania katika miaka yote 10 ya urais wa Mkapa na kwa sasa ndiye mwanasiasa anayeongoza kwa kushikilia wadhifa huo kwa muda mrefu kuliko mwingine yeyote.
Tangu Sumaye ajiunge na kambi ya Upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kumekuwa na taarifa kwamba uhusiano wake na Mkapa ulikuwa umezorota na kwamba maneno makali yaliyotumiwa na rais huyo wa Awamu ya Tatu yalikuwa yamemlenga Sumaye moja kwa moja.
Agosti 27 mwaka huu pia, wakati Mkapa alipokuwa akiadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya ndoa yake na mama Anna Mkapa, Sumaye hakuhudhuria tukio hilo ingawa lilihudhuriwa na Edward Lowassa ambaye alikuwa waziri mkuu baada ya Sumaye.
Hata hivyo, katika mahojiano yake na Raia Mwema wiki hii, Sumaye alisema wanaosema kwamba uhusiano wake na Mkapa umezorota ni “watunga maneno” na kwamba hana tatizo lolote na bosi wake huyo.
“ Ngoja nikwambie bwana. Wanaosema mimi na Mkapa tuna matatizo ni watunga maneno ambao wanazungumza tu bila kufanya utafiti. Mimi na Mkapa hatuna uadui wala uhasama.
“ Hata kwenye hiyo Jubilei yake alinialika lakini kwa bahati mbaya mimi nilikuwa safarini Malaysia na ndiyo maana nikashindwa kuhudhuria. Kama ningekuwa hapa nchini ningeenda tu kwenye ile sherehe,” alisema Sumaye kwa msisitizo.
Akizungumzia maisha yake mapya kama mmoja wa viongozi wa Upinzani nchini, Sumaye alisema hadi sasa maisha yake yako kama zamani na kwamba hapati shida wala misukosuko ya aina yoyote.
Katika mahojiano aliyowahi kufanya na Raia Mwema huko nyuma, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, aliwahi kueleza kuhusu namna kujiunga kwake na Upinzani kulivyomletea misukosuko kazini na kumpotezea marafiki serikali.
Hata hivyo, kwa upande wake, Sumaye alisema hadi sasa hajafanyiwa vitimbi vya aina yoyote wala kunyimwa haki zake kama waziri mkuu mstaafu; hata kama sasa yeye ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“ Kama ni matatizo nina matatizo mengine tu ambayo ninayo lakini siwezi kuyasema sasa kwa sababu wakati wake bado. Hata hivyo kwa maana ya maisha naishi maisha yangu yaleyale ya kawaida.
“ Sijaona kama nanyanyaswa. Sijanyimwa jambo ambalo nastahili kupata na ninaendelea na marafiki zangu ambao nimekuwa nao kwa muda wote. Kwa kweli naishi maisha yangu ya kawaida kabisa,” alisema Sumaye.
Wakati anachaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1995, Sumaye alikuwa ametoka kuwa waziri wa kilimo, chakula na ushirika na katika umri wa miaka 45 aliokuwa nao wakati huo, alikuwa mmoja wa mawaziri wakuu wenye umri mdogo katika historia ya Tanzania.
0 comments:
Post a Comment