TIMU ya soka ya wavulana ya Ilala Boys jana imetwaa ubingwa wa michuano ya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Aitel Rising Stars (ARS) kwa kuwafunga Bom Bom FC mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa wasichana timu ya Simba Queens ndio iliyotawazwa mabingwa kwa kuishinda timu ya Ilala Queens kwa mabao 5-0 katika mchezo mkali uliovuta hisia za watazamaji waliojitokeza kushuhudia mtanange huo jana.
Katika mchezo wa wavulana, Ilala Boys walionesha dalili za ushindi mapema baada ya kuanza mchezo kwa mashambulizi mfululizo na walichukua dakika sita kuandika bao la kuongoza likifungwa na Rajabu Ally baada ya kugongeana vyema na mshambuliaji mwenzake Issa Abushiri.
Dakika ya saba ya mchezo huo Ilala Boys waliandika bao la pili baada kupigwa mpira wa kona na mabeki wa Bom Bom FC kushindwa kuokoa. Bao la tatu lilipatikana dakika ya 42 ya kipindi cha pili baada ya kupigwa mpira mrefu huku mabeki wa Bom Bom wakisimama wakifikiri mfungaji Issa Abushiri ameotea.
Akikabidhi vikombe kwa washindi, Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azzan Zungu aliwataka wachezaji waliochaguliwa kuwakilisha Mkoa wa Ilala vyema kwenye fainali za Taifa za ARS zinazotarajiwa kufanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba mwaka huu.
“Mkoa wa Ilala ulikuwa kila mwaka ukifanya vizuri kwenye mashindano, nina imani nanyi mtaendelea kulinda heshima ya mkoa wetu," alisema Zungu.
Zungu pia alitoa pongezi kwa Kampuni ya Airtel kwa kutoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji vyao vya kandanda.
Naye Meneja Huduma za jamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi alizipongeza timu zote kwa kushiriki na kuwaasa wachezaji kulinda na kuviendeleza vipaji vyao ambavyo ni hazina kwa taifa. Alisema lengo lilikuwa ni kuibua vipaji na kuwaasa vijana ambao hawakuchaguliwa kutokata tamaa na badala yake wajiunge kufanya vizuri mwakani.
Kukamilika kwa michuano hiyo mkoa wa Ilala ndio kunafunga pazia la ARS ngazi ya mkoa huo iliyoanza kutimua vumbi mwezi uliopita.
Mashindano ya Airtel Rising Stars ambayo mwaka huu yanashirikisha mikoa ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Morogoro, Mbeya, Mwanza, Zanzibar, Lindi na Arusha zinatarajiwa kuingia kwenye hatua nyeti ya fainali za Taifa iliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, kuanzia Septemba 6 hadi 11 mwaka huu
0 comments:
Post a Comment